Waziri Kakunda aitaka Veta kuwekeza kwenye teknolojia ya kisasa
WAZIRI wa Viwanda Biashara na Uwekezaji Joseph Kakunda amesema ni vyema Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kuanza kuwekeza katika kubuni teknolojia za kisasa na kuzalisha mashine za kurahisisha shughuli za viwanda nchini.
Kakunda aliyasema hayo alipotembelea banda VETA katika Maonesho ya Tatu ya Bidhaa za Viwanda Tanzania yanayofanyika katika Viwanja vya Mwl. J.K. Nyerere-Sabasaba jijini Dar es Salaam.
Amesema kutokana na mkakati wa serikali kwenda katika uchumi wa kati kupitia viwanda, VETA inawajibu wa kuzalisha nguvu kazi yenye uwezo wa kubuni teknolojia ambazo zitarahisisha kufanya uchakataji wa malighafi zinazolishwa nchini.
Kakunda amesema kuwa mali ghafi zikichakatwa nchini zitasaidia kuongeza mnyororo wa thamani wa malighafi hizo na hatimaye kuwasiadia wakulima kunufaika na kilimo wanachokifanya.
“VETA mna nafasi kubwa nchini katika maendeleo ya viwanda na serikali inawategemea katika uzalishaji wa teknolojia na nguvu kazi ili kusaidia kusukuma maendeleo hayo,” alisema.
Maonesho ya tatu ya bidhaa za viwanda yanafanyika katika viwanja vya Sabasaba kuanzia tarehe 5 hadi 9 Desemba 2018

No comments